Rais wa Kenya William Ruto aliitisha kikao maalum cha baraza la mawaziri siku ya Jumanne kujadili hatua za kukabiliana na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya karibu watu 170 na wengine 185,000 kuyahama makazi yao tangu Machi, ofisi yake ilisema.
Mvua kubwa kuliko kawaida za masika, zikichangiwa na hali ya hewa ya El Nino, zimeharibu nchi hiyo ya Afrika Mashariki, na kumeza vijiji na kutishia kusababisha uharibifu zaidi katika wiki zijazo.
Katika kisa kibaya zaidi ambacho kiliwauwa karibu wanakijiji 50, bwawa la muda lilipasuka katika Bonde la Ufa kabla ya mapambazuko ya Jumatatu, na kusababisha mafuriko ya maji na matope kumwagika chini ya kilima na kumeza kila kitu kwenye njia yake.
Janga hilo lilikuwa tukio baya zaidi nchini tangu kuanza kwa msimu wa mvua.
Kufikia sasa, watu 169 wamekufa katika majanga yanayohusiana na mafuriko, kulingana na data ya serikali.
Baraza la mawaziri “litajadili hatua za ziada” kushughulikia mzozo huo, Ruto alisema Jumatatu kando ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika na Benki ya Dunia katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.