Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali tayari imeshampata Mkandarasi na kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41 kwa kiwango cha lami.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongezwa kwa ujenzi wa kilometa 10 katika barabara hiyo ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji kwa kuinganisha na kipande kilichobakia cha Kimbiji hadi Cheka kwa kiwango cha lami.
Bashungwa amezungumza hayo Aprili 29, 2024 Wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi ya kukagua athari za miundombinu ya barabara na madaraja zilizotokana na mvua za El-Nino na kujionea hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS).
“Nilivyokuja Kigamboni kukagua barabara hii ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji tulikuwa hatujasaini mkataba, nitumia nafasi hii kuwataarifu kuwa tayari tumesaini mkataba na sasa Mkandarasi anaendelea kuleta mitambo eneo la kazi ili mvua itakapokatika aweze kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami na haitakuwa kilometa 41 tena bali 51 kwani tunaiunganisha na kipande kilichobakia cha Cheka hadi Kimbiji”, amesema Bashungwa.