Waziri wa Madini, Antony Mavunde Leo akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 amesema kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na madini mkakati ambayo uhitaji wake ni mkubwa kwenye nishati safi na salama na teknolojia nyingine za kisasa duniani.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema uhitaji wa madini hayo unatokana na utekelezaji wa azimio la pamoja la dunia la kupunguza hewa ya ukaa ifikapo 2050 (Net Zero Emission).
Ametaja miongoni mwa madini mkakati yanayopatikana nchini ni pamoja na lithium, cobalt, nikeli, shaba, aluminium, zinki, kinywe pamoja na rare earth elements (REE).
Amesema ili nchi yetu iweze kunufaika na madini hayo, Wizara imeandaa mkakati wa uendelezaji wa madini muhimu na madini mkakati hapa nchini.
“Mkakati huo unalenga kuhakikisha kwamba madini hayo yanaongezwa thamani hapa nchini ikiwemo kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika soko kama vile betri za magari ya umeme na hivyo kuongeza manufaa kwa nchi ikiwemo kuongeza mapato ya serikali na ajira kwa watanzania,” amesema.
Amesema ili kuongeza manufaa yatokanayo na madini muhimu na madini mkakati, kwa mara ya kwanza kitajengwa kiwanda kikubwa na cha kisasa cha usafishaji na uongezaji thamani madini hayo, Buzwagi Wilaya ya Kahama.