Serikali ya Russia imelegeza masharti ya kanuni zinazohusu maombi ya raia wa kigeni wanaoomba uraia, na itaruhusu mwanamke wa Kiislamu kutumia picha za paspoti zinazomuonesha akiwa amevaa vazi la staha la Kiislamu la Hijabu.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo.
Sheria hiyo mpya itaanza kutumika Mei 5, siku kumi baada ya kuchapishwa.
Taarifa hiyo imefafanua kwa kusema, “katika hali ambapo imani za kidini za mwombaji hazimruhusu kujitokeza mbele ya maajinabi pasi na kufunika kichwa, zitolewe picha zilizofunika kichwa lakini zisizoziba mviringo wa uso” .
Hata hivyo, taarifa hiyo imeongeza kuwa, picha zilizo na mitandio ambayo inaficha kikamilifu au kwa kiasi fulani kidevu cha mwombaji hazitakubaliwa.
Mamlaka za Russia tayari zimewaruhusu raia wake kutumia picha wakiwa wamevalia hijabu wanapotuma maombi ya pasipoti, leseni za udereva, vibali vya kufanyia kazi na hatimiliki.
Biysultan Khamzaev, mjumbe wa Kamati ya Usalama na Kupambana na Ufisadi ya Bunge la nchi hiyo Duma ameliambia gazeti la bunge hilo kwamba, sheria hizo mpya zitawaruhusu waumini kutekeleza mafundisho yao ya kidini, na kuhakikisha pia usalama wa serikali, kwa sababu kama zilivyo data zingine, sura inahitajika ili mifumo ya ufuatiliaji ya video iweze kumtambua mtu.