WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani, utakuwa huru bila kuwapo vihatarishi vya uvunjifu wa amani.
Masauni amesema kila mtu atapata haki yake ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa bila kuwapo kwa vihatarishi vya amani katika maeneo yote uchaguzi utakapofanyika.
Ametoa kauli hiyo baada ya kufungua Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato jijini, Dodoma.
“Niwahakikishie wananchi, tumejipanga vizuri kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani. Niwaombe Watanzania watege masikio kuelekea bajeti ya wizara ambayo tutaiwasilisha bungeni katikati ya mwezi unaokuja.
“Tunaenda kuboresha takribani kila sehemu katika vyombo vyetu vya usalama hasa Jeshi la Polisi, tunaenda kuliboresha katika kila sehemu ikiwamo vifaa na mambo mengine mbalimbali,” amesema.
Waziri Masauni amewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kuhusu uchaguzi ujao kwa kuwa Jeshi la Polisi liko vizuri kuhakikisha demokrasia inaendelea kutekelezwa katika misingi ya amani na utulivu na watu wanachagua na kuchaguliwa bila bughudha yoyote, huku nchi ikiendelea kubaki salama.
Akizungumzia chaguzi hizo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus Wambura, amempongeza Waziri Masauni kwa kusimamia ongezeko la bajeti kwa wizara na vyombo vyake.
Amesema ongezeko hilo linakwenda kuboresha utendaji kazi hasa wa Jeshi la Polisi kuelekea pia uchaguzi wa Serikali za Mita na Uchaguzi Mkuu.