Njaa na utapiamlo vinaenea kote nchini Sudan, mwaka moja tangu kuzuka kwa vita kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Usaiidizi wa Haraka (RSF) huku ikiwa hakuna dalili ya vita kusitishwa hivi karibuni.
Katika baadhi ya kambi za watu waliokoseshwa makaazi huko Darfur Kaskazini, wakaazi, madaktari na wafanyakazi wa misaada wanasema kuwa, watu wamelazimika kula udongo na majani.
Kwa mujibu wa shirika linaloangazia usalama wa chakula, IPC, takriban watu milioni 18 nchini Sudan, ikiwa ni zaidi ya theluthi moja ya watu, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Wakati huo huo zaidi ya watu nusu milioni wanalazimika kuvuka mpaka karibu kila siku na kuingia Sudan Kusini kwa kutumia vivuko mbalimbali vya mpaka.
Idadi ya wanaokimbia inazidi kuongezeka huku mzozo ukiendelea, watu wengi wanafika wakiwa wamedhoofika, wakiw na njaa na waliokata tamaa.