Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya Tanzania umeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya Nchi ambapo hadi kufika saa tatu usiku wa tarehe 02 Mei 2024 kilikuwa umbali wa takriban Kilomita 402 Mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Taarifa ya TMA imesema nguvu ya kimbunga HIDAYA imeendelea kuimarika na kuwa kubwa zaidi hadi kufikia usiku huo kasi ya upepo katika kimbunga iliongezeka na kufika kilometa 110 kwa saa ambapo inatarajiwa kuendelea kuimarika zaidi katika kipindi cha saa 24 kutoka muda huo.
“Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga “HIDAYA” kuendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania na kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 mwezi Mei 2024 ambapo kinatarajiwa kupungua nguvu baada ya tarehe 6 Mei 2024” ——— imeeleza taarifa ya TMA.
Uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu na pwani ya Tanzania unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani.
Vipindi vya mvua nyepesi na upepo wa wastani tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Mtwara huku ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vikitarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 Mei 2024.