Waziri wa Masuala ya Dharura nchini Rwanda Albert Murasira amesema, athari zilizotokana na mvua kubwa yakiwemo maporomoko ya udongo na radi, zimesababisha vifo vya watu 50 na wengine 79 kujeruhiwa nchini humo katika miezi miwili iliyopita.
Murasira amesema kuuwa, watu 12 wamefariki kwa kupigwa na radi huku wengine wakifariki kwa kuangukiwa na nyumba zao mbovu.
Waziri huyo aidha amesema, serikali imewahamisha wakazi karibu elfu 5 kutoka maeneo yenye hatari kubwa hadi maeneo salama kote nchini.
Maafa hayo pia yameharibu miundombinu, ikiwemo nyumba, madaraja, majengo ya shule, mitandao ya barabara pamoja na mashamba.
Wakati huo huo, Rwanda, imetangaza kwamba kutokana na mvua kubwa iliyotabiriwa katika wiki ya kwanza ya Mei, baadhi ya mito inaweza kuvunja kingo zake na kusababisha mafuriko katika jamii.
Tahadhari hiyo imetolewa na Bodi ya Rasilimali za Maji ya Rwanda (RWB), na kusisitiza kuwa, mito inayoweza kusababisha mafuriko ni pamoja na Mto Sebeya, Karambo, Nyabahanga, Kabirizi, Nyabarongo, Mwogo, Mukungwa, Rubyiro, Cyagara, pamoja na mito ya Ukanda wa Virunga.