Rais wa Togo Faure Gnassingbe ametia saini katiba mpya yenye utata ambayo itaondoa uchaguzi wa rais, taarifa kutoka ofisi yake ilisema Jumatatu jioni. Ni hatua ambayo wapinzani wanasema itamruhusu kuongeza muda wa utawala wa familia yake wa miongo sita.
Chini ya sheria hiyo mpya, bunge litakuwa na mamlaka ya kuchagua rais, na kuondoa uchaguzi wa moja kwa moja. Tume ya uchaguzi siku ya Jumamosi ilitangaza kuwa chama tawala cha Gnassingbe kimepata viti vingi katika bunge la taifa hilo la Afrika Magharibi.
Kabla ya upigaji kura, serikali ilipiga marufuku maandamano ya kupinga katiba mpya inayopendekezwa na kuwakamata viongozi wa upinzani.
Tume ya uchaguzi ilipiga marufuku Kanisa Katoliki kupeleka waangalizi wa uchaguzi.
Katikati ya Aprili, mwandishi wa habari wa Ufaransa ambaye alifika kuripoti uchaguzi alikamatwa, kushambuliwa na kufukuzwa.
Mdhibiti wa vyombo vya habari nchini Togo baadaye alisimamisha mchakato wa kuwaidhinisha waandishi wa habari wa kigeni.