Mahakama ya Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela, Paulo John (23) Mkazi wa Mapea Magugu na Athumani Misanya (31) Mkazi wa Marire baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za serikli ikiwemo kichwa cha Twiga.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu wa Mahakama hiyo, Victor Kimario baada ya kusikiliza hoja za pande zote.
Katika hukumu hiyo amesema amejiridhisha pasina kuacha shaka juu ya ushahidi wa upande wa Jamhuri, hivyo kwa kuzingatia kuwa wakosaji ni wa mara ya kwanza licha ya kuwa vijana wadogo lakini wametumia nguvu zao vibaya kuihujumu Serikali hivyo amewahukumu kwenda Jela miaka 20 kila mmoja huku vifaa vilivyotumika kubebea nyara hizo(Ndoo na Pikipiki) kutaifishwa huku haki ya kukata rufaa ikiwa wazi ndani ya siku 30 kuanzia leo.
Awali waendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) Getrude Kariongi na Shaidu Kajwangya wakishirikiana na wakili Mwanaidi Chuma wamesema washtakiwa hao wanadaiwa kutenda Kosa hilo 02/02/2024 katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge
Wamesema washtakiwa hao walikutwa na Kichwa cha Twiga,Mkia,ngozi pamoja na nyama vikiwa kwenye ndoo huku wakitumia usafiri wa pikipiki ambapo thamani ya Twiga huyo ikiwa ni zaidi ya shilingi Milioni 50,ambapo wameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu ili kufikisha ujumbe kwa jamii na watu wenye kufanya makosa ya ujangili ili kukomesha vitendo hivyo kwani Mnyama Twiga ni nembo ya Taifa lakini pia ni kivutio cha Utalii na kuiwezesha nchi kupata Mapato.
Kwa upande wake Wakili wa utetezi Festo Jackson ameiomba mahakama Kwa kuwa watuhumiwa hao ni wakosaji wa mara ya kwanza na Umri wao bado ni mdogo na wapo na wategemezi wanao wategemea hivyo Mahakama iwaonee huruma na kuwapunguzia adhabu.