Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme itakayoboresha upatikanaji umeme mkoani Songwe ikiwemo ujenzi wa kituo cha umeme na switching station .
Naibu Waziri Kapinga amesema hayo tarehe 8 Mei, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Mbozi, Mhe. George Mwenisongole aliyetaka kufahamu ni lini ujenzi wa Kituo cha upoza Umeme Kakozi, Tunduma utaanza.
Akijibu swali hilo Mhe. Kapinga alisema “Serikali kupitia mradi wa TAZA unaotekelezwa na TANESCO ipo katika hatua za awali za ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nkangamo (Tunduma) kilichopo takribani kilomita 28 kutoka Kijiji cha Kakozi, Mbozi. Ujenzi wa kituo hiki unatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo kwa sasa mkataba kati ya TANESCO na mkandarasi atakayejenga kituo hiki tayari umeshasainiwa.”
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa kituo hicho cha Nkangamo (Tunduma) kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Kijiji cha Kakozi na maeneo mengine ya Jimbo la Mbozi.
Akizungumzia hali ya upatikanaji umeme kwa ujumla mkoani Songwe, Kapinga amesema kuwa mkoa huo unapata umeme kutoka kituo cha Mwakibete kilichopo mkoani Mbeya ambapo laini hiyo ya umeme ni ndefu sana na kupelekea kutokea kwa changamoto za upatikanaji umeme mkoani Songwe.
Kutokana na hilo amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo ya kujengwa switching station mkoani Songwe pamoja na kituo cha umeme kitakachojengwa kupitia mradi wa TAZA huku uboreshaji wa miundombinu ya umeme ukiendelea.
Akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Mhe. Margaret Sitta aliyetaka kufahamu ni lini kituo cha umeme cha Uhuru kitakamilika, Mhe. Kapinga amesema kituo kipo ukingoni kukamilika na hivyo kuboresha hali ya umeme wilayani Urambo.