Ndege ya Boeing 737 iliyokuwa imebeba watu 85 ilipata ajali kutoka kwenye uwanja wa ndege wa Dakar, mji mkuu wa Senegal, na kuwajeruhi watu 10, taarifa ya waziri wa uchukuzi wa nchi hiyo ilisema katika taarifa yake siku ya Alhamisi.
El Malick Ndiaye, waziri wa uchukuzi, alisema ndege ya Air Sénégal inayoendeshwa na TransAir ilikuwa inaelekea katika mji mkuu wa Mali, Bamako, Jumatano jioni ikiwa na abiria 79, marubani wawili na wafanyakazi wanne wa vyumba vya ndege.
Majeruhi walikuwa wakitibiwa hospitalini, huku wengine walionusurika wakipelekwa hotelini kupumzika.
Ndege hiyo ilitoka kwenye njia kabla ya kupaa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Blaise Diagne, ripoti ya AFP ikinukuu taarifa rasmi.
Ajali hiyo ya Dakar ni ya hivi punde zaidi katika mfululizo wa matukio yanayokumba ndege za Boeing. Haya yanajiri siku moja tu baada ya ndege ya mizigo ya Boeing kulazimika kutua kwenye pua yake mjini Istanbul baada ya gia yake ya kutua ya mbele kuanguka.