Hatua hii iliafikiwa baada ya serikali na Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini (KMPDU) kukitia saini mkataba wa kurejea kazini.
Makubaliano hayo yalifanikishwa na mikutano ya maridhiano siku Jumanne kati ya KMPDU na serikali kupitia Baraza la Magavana (CoG) pamoja na Wizara ya Afya.
Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah, akizungumza baada ya kutia saini makubaliano na serikali siku ya Jumatano jioni, alisema Baraza la Kitaifa la muungano huo linaunga mkono maazimio yaliyopelekea kusitishwa kwa mgomo.
“Tumetia saini mkataba wa kurejea kazini na muungano umesitisha mgomo,” Susan Nakhumicha, waziri wa afya alisema.
Malimbikizi ya madaktari yalitokana na makubaliano ya pamoja ya 2017 (CBA), KMPDU ilisema. Madaktari pia walikuwa wakitaka kupatiwa bima ya matibabu iliyoboreshwa kwa ajili yao na familia zao.
“Jambo moja lazima tumhakikishie kila mtu, kila daktari ni kwamba haki za wafanyikazi kama ilivyoandikwa katika makubaliano ya mazungumzo ya pamoja ambayo yametiwa saini ni kwamba ni matakatifu, tutajitahidi kila wakati kulinda hilo,” Dhavji Atellah, katibu mkuu wa KMPDU, alisema.
Kumalizika kwa mgomo huo kutatoa afueni kwa wanaotafuta huduma katika serikali za umma, hasa kufuatia mvua kubwa inayonyesha na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu 257 tangu mwezi Machi, na kusababisha watu 293,661 kukosa makazi.