Afisa mwandamizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ametahadharisha kuwa, dunia ipo katika hatari ya kukumbwa na janga la matatizo ya afya ya akili.
Hans Kluge, Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya ametoa tahadhari hiyo katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu na kueleza kuwa, “Changamoto za afya akili, ndilo janga lijalo duniani.”
Kluge amebainisha kuwa, janga la COVID-19 limekuwa na athari kubwa kwa afya ya akili ulimwenguni kote hasa miongoni mwa vijana, na kwamba lazima hatua zichukuliwe ili kukomesha ukosefu wa usawa uliofichuliwa na tandavu hiyo.
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa WHO amekumbusha kuwa, karibu asilimia 20 ya watoto na vijana duniani wanasumbuliwa na changamoto za afya ya akili, na kujiua ndio sababu ya pili ya vifo kati ya watoto wa miaka 15-29.
Ripoti iliyochapishwa Agosti 28, 2023 na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha kuwa, zaidi ya watu 700,000 hujitoa uhai kila mwaka kote duniani; aghalabu yao kutokana na msongo wa mawazo na matatizo mengine ya kisaikolojia.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, afya ya akili imekuwa changamoto kubwa ya afya ya umma na ya kijamii katika nchi mbalimbali duniani, zikiwemo zilizostawi na kuendelea.