Rais William Ruto wa Kenya ametangaza kuwa siku ya leo Ijumaa kuwa ni siku ya mapumziko ili kuwaomboleza watu 238 waliopoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyoiathiri nchi hiyo.
Rais Ruto jana alitangaza pia itakuwa siku ya kupanda miti ili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kenya pamoja na maeneo mengine ya Afrika Mashariki yameathiriwa pakubwa na mafuriko. Watu zaidi ya 235,000 wamelazimika kuhama makazi yao na sasa makumi ya watu wanaishi makambini.
Rais Ruto pia ametangaza kufunguliwa shule kote nchini ifikapo tarehe 13 mwezi huu wa Mei, baada ya kuchelewa kwa wiki mbili kutokana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko na mamia ya shule kufungwa.
Serikali ya Kenya imesema kuwa shule zaidi ya 1,000 zimeathiriwa na mvua kubwa na kuwa tayari imetenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hizo.