Halmashauri ya Wilaya ya Madaba wafanya ziara ya mafunzo Wilayani Mufindi kujionea shughuli za upandaji miti uchakataji wa mazao ya misitu na uhifadhi wa misitu na mazingira.
Kwa muda wa siku mbili Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba iliyopo Mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia Shamba la Miti Wino wamefanya ziara ya mafunzo katika Shamba la Miti Sao Hill lengo ikiwa ni kujifunza kuhusu na uzalishaji wa mazao ya misitu.
Ziara hiyo ilihusisha kiongozi wa msafara huo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Wilman Kapenjama Ndile, Madiwani, wenyeviti na Wahifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – Shamba la Miti Wino wakiongozwa na Mhifadhi Mkuu Glory Fortunatus, ambapo katika ziara hiyo walitembelea viwanda mbalimbali vinavyozalisha malighafi zitokanazo na mazao ya misitu.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Songea amesema kuwa ziara hiyo imefanyika kwa malengo matatu ambayo ni kujifunza kuhusu upandaji wa miti kuanzia hatua ya mwanzo mpaka uvunaji, uchakataji wa mazao ya misitu katika viwanda na manufaa yake, lakini pia kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto za uendelezaji wa rasilimali za misitu kama vile kukabiliana na majanga ya moto wa misituni.
“Nitoe pongezi zangu kwa TFS kuhusu utoaji wa elimu ya namna ya utunzaji wa miti na mazingira kwa ujumla, lakini pia tumeona manufaa mengi ikiwa ni pamoja na makusanyo makubwa ya mapato kwa halmashauri zote mbili za Wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji Mafinga na utoaji wa ajira kwa vijana na jamii inayozunguka maeneo ya shamba zitokanazo uwepo wa mazao ya misitu”, Alisema Mkuu wa Wilaya
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mhe. Teofanes Mlelwa amesema kuwa wamejifunza mengi na kubwa zaidi ni uwepo wa kiwanda ambacho kinatumia malighafi yote ya mti ikiwa ni mabaki ya miti katika utengenezaji wa bidhaa.