Mtanzania, Denis Mfumbulwa (44) mkazi wa Goba Kulangwa, Dar es Salaam anatarajiwa kurudishwa tena katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, Mei 15, 2024 katika kesi inayomkabili ya kujipatia huduma kwa njia ya udanganyifu.
Kwa mara ya kwanza Mfumbulwa alifikishwa mahakamani hapo Mei 13, 2024 akikabiliwa na mashtaka hayo ambayo alisomewa mbele ya Hakimu Gladness Njau.
Karani wa mahakama hiyo, Aurelia Bahati alidai kuwa Machi 6, 2022 hadi Machi 28, 2024 kwa nyakati tofauti katika Hoteli ya Serena Mtaa wa Ohio Wilaya ya Ilala, Dar es salaam mshtakiwa alijipatia huduma ya malazi na chakula yenye thamani ya Shilingi Milioni 21,491,866.97/= bila kulipa mali ya mlalamikaji Desdery Dotto na hatimaye kutoweka huku akijua kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili alikana kutenda kosa hilo. Hata hivyo, mshtakiwa alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo;
Ni kuwa na wadhamini wawili wenye barua zinazowatambulisha na mmoja kati yao kusaini bondi ya Sh milioni 10. Hakimu Njau aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 15, mwaka huu.