Waziri Mkuu wa Israel anakadiria kuwa karibu “wapiganaji 14,000 wameuawa na pengine takriban raia 16,000”, jumla ya watu 30,000 waliuawa katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita.
Waziri Mkuu wa Israel anataja kwa mara ya kwanza idadi ya vifo vya watu 30,000 katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, takriban nusu yao ni “wapiganaji wa Hamas”, katika podikasti iliyotolewa siku ya Jumapili hii, Mei 12.
Takriban “wapiganaji 14,000 waliuawa na pengine takriban raia 16,000 waliuawa,” Benjamin Netanyahu amesema.
Hadi sasa, idadi ya vifo huko Gaza inatolewa haswa na Wizara ya Afya ya Hamas, iliyoko madarakani huko Gaza. Inakadiria kuwa zaidi ya watu 35,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamefariki tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel kufuatia shambulizi la Oktoba 7.
Benjamin Netanyahu amesisitiza kuwa rekodi yake kwa ujumla ilikuwa chini kuliko ile iliyotangazwa na Hamas. Takwimu zinazohesabu idadi ya vifo huko Gaza ni vigumu kuthibitisha. Hivi majuzi, Umoja wa Mataifa uliacha kuripoti takwimu kutoka kwa ofisi ya vyombo vya habari vya serikali ya Gaza, ambazo zilionekana kuwa haziendani. Shirika hilo sasa linatumia takwimu kutoka Wizara ya Afya ya Hamas.