Mbunge wa Jimbo la Morogoro MJINI Mhe. Dokta Abulaziz Abood ametoa msaada wa Madawati yenye thamani ya zaidi ya Tsh. Mil. 25 katika Shule ya Sekondari ya Mazimbu Manispaa ya Morogoro kama sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake kufuatia ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya Shule mpya zilizojengwa katika Halmashauri hiyo .
Zoezi hilo la kukabidhi madawati katika Shule hiyo limefanyika kufuatia ziara ya Mhe Abood alioifanya Januari 10 Mwaka huu kwenye Shule hiyo na kujionea upungufu mkubwa wa Madawati pamoja na Viti, ambapo kwa kiasi kikubwa aliona namna wanafunzi wa Shule hiyo Mpya wanavyokumbana na changamoto ya kukaa chini ili waweze kujifunza kwa utulivu na hiyvo, kuamua kupeleka Madawati hayo ambayo ni Meza 310 pamoja na viti 310 ili kuondoa changamoto hiyo.
Mhe Abood ameweka wazi kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika kuimarisha miundombinu ya elimu kwa kuendeleza ujenzi wa Shule za Sekondari na Msingi nchini kote ili elimu yenye ubora iweze kutolewa kwa kiwango chenye uhakika na hatimaye Taifa liweze kushindana na kuendana na vigezo vya ushindani katika soko la ajira.
Aidha,Mhe Abood amefafanua kwamba, ujenzi wa madarasa ni jambo moja na kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais kwa kuweka madawati ili watoto waweza kupata hari ya kusoma ni jambo lingine, hivyo kama Mbunge ameliona hilo na kuamua kutengeneza Meza pamoja na Viti vyenye uwezo wa kutosha kuhudumia wanafunzi na madarasa zaidi 6, kwa lengo la kuwafanya walimu wafundishe vema na wanafunzi wajifunze kwa utulivu mkubwa na kuleta matokeo chanya ya kielimu kwenye Manispaa hiyo na Taifa kwa ujumla.
“Nilikuja hapa katika ziara yangu ya kushtukiza na nikakutana na changamoto ya madawati, nimekuta wanafunzi wanakaa chini, nilihisi nina jambo naweza fanya, na ndipo nilipoahidi kuwa nitatoa madawati ili kuondoa changamoto na hatimaye watoto wetu waweze kukaa kwa utulivu, leo nimetekeleza
Amesema Serikali imeshawekeza fedha kwa kutujengea Madarasa ya Sekondari na Msingi kwa gharama kubwa, sasa palipobaki na sisi lazima tuoneshe kugusa na hili, taratibu hadi tutamaliza lakini kwa sasa haya tuoleta leo yatapunguza kwa kiasi kikubwa kero ya Madawati kwenye Shule hii.
Katika hatua nyingine, Mhe Abood amewahakikishia wananchi wa jimbo hilo kuwa, wapo baadhi ya wananchi ambao hawana uwezo wa kwenda na kuwasilisha kero Ofisini kwake hivyo, ameweka utaratibu mpya kupitia kwa Wenyeviti wa Mitaa na Watendaji wa Serikali ili kufika moja kwa moja kwenye eneo analoishi mwananchi husika na kusikiliza kero yake papo hapo kwani yeye ni Mbunge aliochaguliwa na watu wote ili kuwatumikia wananchi hao kwa kasi kubwa, Moyo mmoja, Hari na mali na kwa nguvu zake zote na kamwe kasi ya kuwatumikia na kusimamia miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayohusu Jimbo hilo haitapungua.
Kwa upande Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo ambaye pia ni diwani wa Kata ya Mazimbu Mhe. Pascal Kihanga amebainisha kuwa, Mbunge Abood amekuwa msaada mkubwa ndani na nje ya Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo na kupelekea Baraza hilo kufanikiwa kutengeneza madawati zaidi ya 5000 ambayo yanatarajiwa kusambazwa katika Shule zote mpya zilizopo kwenye Manispaa hiyo ili kumaliza kabisa tatizo hilo.
Akiliwakilisha wazazi wa Shule hiyo, ndugu Hezron Njau, pamoja na pongezi kubwa kwa Mbunge huyo, ndugu Hezron amemuomba Mbunge Abood kushughulikia maagizo ambayo aliyatoa wakati wa Ziara yake ya Januari 10 Mwaka huu kuhusu urekebishaji wa Sakafu kwa baadhi ya madarasa, pia kuongezwa kwa walimu wa somo la Hesabu na Fizikia kwa lengo la kusaidia kuzalisha wanasayansi Shuleni hapo.