Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia vituo vya utafiti vya Ukiriguru (Mwanza) na Tumbi (Tabora) kwa kushirikiana na watafiti kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo ukanda wa Kitropiki (IITA) wametoa mafunzo kwa baadhi ya wakulima wa mkoa wa Tabora juu ya kanuni bora za kilimo cha zao la muhogo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tano katika vijiji 10 vya Wilaya za Uyui, Urambo na Kaliua na kuhudhuriwa na wakulima 516, yalilenga kuwawezesha wakulima kutambua magonjwa yanayoathiri muhogo na kufahamu matumizi ya mbegu bora zinazohimili magonjwa hasa Batobato na Michirizi kahawia. Magonjwa hayo husababishwa na virusi na kupunguza mavuno na ubora wa muhogo.
Baadhi ya wakulima waliohudhuria mafunzo hayo wamesema awali walikuwa hawayafahamu magonjwa hayo na namna ya kukabiliana nayo, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuzalisha muhogo kwa tija.
“Nilikuwa nakiona tu majani yanajikunja, lakini pia mti unakuwa wa kijivu kijivu. Ila kinachosababisha sikijui, nilifikiri kwamba labda ni hali ya hewa. Kitu nilichojifunza ni kwamba magonjwa hayo ndiyo yaliyokuwa yanasababisha nisipate mavuno ya kutosha.” Amesema Joseph Tadeo mkazi wa kijiji cha Usimba, Kaliua.
Naye Yassin Habibu mkazi wa kijiji cha Ulasa kilichopo Wilaya ya Urambo amesema kwa makadirio msimu wa mavuno ukifika alikuwa akipata kati ya mifuko mitano hadi kumi kwa eka moja, kutokana na kupanda mbegu zenye uwezo mdogo wa kuhimili magonjwa.
“Lakini sasa hapa naambiwa kwa hekta moja unapata kama tani 30 ama tumepiga hesabu hapo unapata kwa eka tani 12, kwahiyo inabidi tufanyie kazi ili tuone labda tunaweza kukipenda zaidi kilimo cha muhogo.”
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mafunzo yaliyoanza tarehe 9 hadi 14 mwezi Mei, Mtafiti msaidizi katika zao la Muhogo kutoka TARI Ukiriguru Bi Maria Augustine amesema mwitikio umekuwa wa kuridhisha na wakulima wamefahamishwa pia juu ya uwepo wa mbegu bora zilizofanyiwa utafiti ambazo mbali na kuwa na uwezo mkubwa wa kuvumilia magonjwa, pia zinatoa mavuno mengi tofauti na mbegu za asili.
“Tumekuja kwa ajili ya kuwafahamisha wakulima kwamba kuna wakulima ambao tumeshawafundisha na wanajua jinsi ya kulima na kuzalisha mbegu bora kama TARICASS1, TARICASS2, TARICASS3, TARICASS4, MKURANGA1 na Kiroba ambazo tumezitafiti kutoka kwenye taasisi yetu. Kwahiyo kuna wakulima ambao wameshapata mafunzo na wanazalisha ambao watawauzia wakulima wadogo wadogo waliopo kwenye maeneo haya. Kwahiyo wakishajua ni wakulima gani wanazalisha mbegu inakuwa ni rahisi kwao kuliko kufuata mbegu kwenye taasisi moja kwa moja.” Amesema.