SERIKALI imesema itafunga kamera kwenye maeneo maalum nchini ili kunasa wahalifu.
Maeneo hayo ni pamoja na ya viwanda, biashara, mikusanyiko ya umma, barabara za miji, hoteli na huduma za jamii.
Ni mkakati uliobainishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Amesema mkakati huo utatekelezwa kupitia Mradi wa Miji Salama unaolenga kuboresha mifumo ya usalama nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao unaimarishwa.
“Katika utekelezaji mradi huo, jumla ya kamera 6,500 zenye teknolojia ya akili bandia zinatarajiwa kufungwa katika maeneo ya viwanda, biashara, mikusanyiko ya umma, barabara za miji, hoteli na huduma za jamii.
“Mradi utaanza kutekelezwa mwaka 2024/25 katika majiji ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza. Utatekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani 145,200,000 kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE),” amesema.
Waziri Masauni ametaja maeneo mengine ya kipaumbele mwaka ujao wa fedha ni pamoja na kuendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai; kukamilisha, kuendeleza na kuanza ujenzi wa ofisi, vituo na makazi ya askari na kuongeza vitendea kazi vya kisasa katika kutoa huduma ikiwamo magari, pikipiki, boti na helkopta.
Amesema wizara yake pia itaanza utekelezaji miradi ya kimkakati ikiwamo Mradi wa Ukaguzi wa Magari wa Lazima, Mradi wa Udhibiti wa Barabara Kuu.