MAHAKAMA ya juu ya makosa ya jinai nchini Uswisi, imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Gambia Ousman Sonko kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu yaliyotendwa enzi ya utawala wa dikteta Yahya Jammeh.
Sonko mwenye umri wa miaka 55 ametiwa hatiani kwa makosa kadhaa yaliyorekodiwa wakati akiwa waziri kati ya mwaka 2000 na 2016. Sonko aliyepachikwa jina la “kamanda wa mateso” alikuwa na dhima ya kusimamia mashambulizi ya kupangwa yaliyotekelezwa na vyombo vya usalama vya Gambia kwa lengo la kuwanyamazisha wapinzani wa utawala wa Jammeh.
DW imeandika kuwa, Kesi yake ilianza kusikilizwa mwezi Januari baada ya kukamatwa nchini Uswisi tangu mwaka 2017 alikokimbilia kujaribu kuomba hifadhi kufuatia kuanguka kwa utawala wa Jammeh.
Kesi yake ilifunguliwa chini ya misingi ya kimataifa ya utoaji haki, ambayo inaruhusu taifa la kigeni kuwashtaki na kuwahukumu watu wanaohusishwa na makosa ya kivitia, mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu.