Hatifungani ya Kijani ya Miundombinu ya Maji Tanga inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) imesajiliwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar Es Salaam (DSE) katika hafla maalumu iliyofanyika Jijini Dodoma katika ofisi za Hazina baada ya mauzo ya Hatifungani hiyo kufanya vizuri kwa 103% zaidi ya lengo.
Akizungumza katika Hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga UWASA, Eng. Geofrey Hilly amewashukuru wadau wote walioshiriki katika kufanikisha uuzaji wa Hatifungani hii na kwa wawekezaji wote walioshiriki katika ununuzi wa hisa na kuahidi kusimamia vyema utekelezaji wa miradi lengwa na kuhakikisha kuwa malipo ya faida kwa wawekezaji yanafanyika kwa wakati.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akitoa salamu za Sekta kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi katika hafla hiyo aliipongeza Tanga UWASA kwa uthubutu huu na kwa kufungua njia na kuwashukuru wadau wote na wawekezaji waliofanikisha jambo hili huku akisisitiza malipo kwa wawekezaji kufanyika kwa wakati.
“Leo nina furaha sana kwa sababu tunaandika historia mpya katika sekta ya Maji nchini, hii ni heshima kubwa sana kwa Wizara ya Maji na Menejimenti ya Tanga UWASA na kikubwa hasa ni kuyaishi maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.
Shukran za dhati ziende kwa wadau wetu wote waliofanikisha jambo hili na kwa wawekezaji wetu wote ndani na nje ya nchi kwa kutuamini na kuwekeza na sisi na tunaahidi kuwa malipo yatafanyika kwa wakati” alisema Mhe. Aweso
Nae Mgeni Rasmi wa Hafla hiyo, Mhe. Innocent Bashungwa (MB), Waziri wa wa Ujenzi akizungumza kwa niaba ya Mhe. Mwigulu Nchemba (MB), Waziri wa Fedha ametoa pongezi kwa Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Tanga UWASA kwa ubunifu huu wa kutafuta chanzo mbadala cha fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo (Altenative Financing) kwani uthubutu huu umeonesha mafanikio mazuri na kuzitaka taasisi za serikali kuiga mfano huu.
“Sote tukubaliane kuwa kupitia Tanga UWASA na kupitia Wizara ya Maji, Serikali imeandika historia mpya kwa kufanya jambo kubwa kama hili, hivyo tunawashikuru sana wadau wote na Wizara ya Fedha kwa kuwa sehemu ya historia hii.
Hii ni kazi nzuri sana inayofanyika kwa usimamizi mzuri na mahili wa Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita Madarakani na Swala hili la Alternative Project Financing ni Nia nzuri na inasimana kama mbadala wa chanzo kingine cha mitaji ya utekelezaji wa miradi ya kuhdumia jamii, tumeona mwitiko wa wawekezaji ambapo tumepata makusanyo ya Shilingi bilioni 54.72 ambapo wawekezaji wa ndani ni 65% na wawekezaji wa nje ni 35%.
Tunatambua michango ya wadau wote walioshiriki katika mchakato huu na nichukue fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Fedha kuzielekeza taasisi nyingine za Serikali kutumia utaratibu huu katika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo”. Alisema Mhe. Bashungwa