Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa limeua takriban magaidi 227 katika operesheni mbalimbali za kupambana na ugaidi zilizofanywa na jeshi hilo katika kote zote za nchi hiyo kwenye kipindi cha wiki iliyopita.
Taarifa ya jana Alkhamisi ya jeshi hilo imeongeza kuwa, magaidi wengine 529 wametiwa mbaroni na wanajeshi hao, ambao walivamia maficho mengi maarufu ya washukiwa hao wa ugaidi ndani ya nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.
Akitoa taarifa hiyo, Edward Buba, msemaji wa jeshi la Nigeria aidha amewaambia waandishi wa habari mjini Abuja kwamba, katika kipindi hicho cha wiki moja, wanajeshi wamefanikiwa kukomboa mateka wasiopungua 253 kutoka mikononi mwa magaidi hao na kuongeza kuwa, jumla ya silaha 231 za aina mbalimbali na risasi 6,441 za aina tofauti pia zimepatikana katika operesheni hizo.
Vitendo vya kigaidi na mashambulio ya kutumia silaha yameshadidi sana nchini Nigeria kiasi kwamba mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei, kwa akali wakulima 30 waliuawa katika shambulizi la genge la wabeba silaha kwenye jimbo la Zamfara la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Msemaji wa Komandi ya Polisi ya Zamfara, Yazid Abubakar alisema katika taarifa yake kuwa, genge hilo la magaidi lilifanya shambulio hilo la umwagaji damu katika maeneo ya Maradun na Tsafe ya jimbo hilo.
Alisema, mwanachuoni maarufu wa Kiislamu, Mallam Makwashi Maradun Mai Jan-Baki ni miongoni mwa zaidi ya watu 10 waliouawa katika shambulizi lililoganywa na magaidi hao kwenye eneo la Maradun.