Takriban Wapalestina 35,303 wameuawa na 79,261 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, wizara ya afya ya Gaza ilisema katika taarifa yake Ijumaa.
Idadi hiyo inajumuisha takriban vifo 31 katika muda wa saa 24 zilizopita, taarifa ya wizara hiyo ilisema, ikiongeza kuwa watu 79,261 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Gaza tangu vita vilipoanza wakati wapiganaji wa Hamas waliposhambulia Israel tarehe 7 Oktoba.
Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas haitofautishi kati ya wapiganaji na wasio wapiganaji.
Mapigano yamepamba moto Ijumaa huko Gaza baada ya Israel kuapa kuzidisha mashambulizi yake ya ardhini huko Rafah licha ya wasiwasi wa kimataifa kwa mamia ya maelfu ya Wapalestina waliokimbia makazi yao katika mji huo wa kusini.
Huku wananchi wa Gaza wakikabiliwa na njaa, jeshi la Marekani lilisema “malori yaliyokuwa yamebeba usaidizi wa kibinadamu yalianza kuhamia ufukweni kupitia gati ya muda” ambayo ilipanga kuwasaidia Wapalestina katika eneo hilo lililozingirwa.