Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika alisema alikuwa akifuatilia matukio katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa “wasiwasi mkubwa” na “analaani vikali” jaribio la mapinduzi huko.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lilisema siku ya Jumapili lilizuia jaribio la mapinduzi karibu na ofisi za Rais Felix Tshisekedi katika mji mkuu Kinshasa unaohusisha “wageni na Wakongo”.
Milio ya risasi ilisikika karibu na eneo la Palais de la Nation ambalo ni ofisi za rais wakati wa jaribio la mapinduzi asubuhi ya Jumapili, kulingana na vyanzo kadhaa.
Mwenyekiti wa Tume ya AU Moussa Faki Mahamat “analaani vikali jaribio hili la mapinduzi na anakaribisha udhibiti wa hali uliotangazwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi,” AU ilisema katika taarifa iliyotolewa Jumapili jioni.
“Anafuraha kuwa viongozi wote wa taasisi za jamhuri wako salama,” ilisema taarifa hiyo.
“Anachukua fursa hii kulaani matumizi yoyote ya nguvu kubadilisha utaratibu wa kikatiba katika nchi yoyote ya Afrika.”