Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa Dkt. Emmanuel Nchimbi amemtaka Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kumaliza changamoto wanazokutana nazo Watumishi ikiwemo kukutana na Jumuiya ya Maafisa wa Rasilimali watu na Utawala ili kuweka utaratibu mzuri utakaosaidia kupunguza Changamoto za watumishi nchini.
Dkt. Nchimbi amezungumza hayo mkoani Morogoro katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Rasilimali watu na mkutano Mkuu wa chama cha Rasilimali watu na Utawala Bora(THRAPA)
“Mmeongelea changamoto kubwa ya kutambuliwa sawa sawa na Wizara inayohusika ya Utumishi, Kupitia kikao hiki namuelekeza Waziri wa Utumishi kukutana na viongozi wenu kuzimaliza changamoto hizi kwa sababu mnapokaa kama chama hamkai kupanga miradi ya Familia zenu mnakaa kupanga mafanikio ambayo yana tija kwenye nchi yetu” amesema Dkt Nchimbi.
Aidha, Dkt Nchimbi amewasisitiza maafisa Rasilimali watu kufanya kazi hiyo kama Wito na kuzingatia haki za Msingi za watumishi wanaowaongoza pamoja na taasisi wanazoziongoza kama Madai, Posho na likizo kwa watumishi.
“Tunalo deni kubwa la kutumikia watu hivyo tujue dhamana tulizonazo zinazohusisha haki za wanaowaongoza kwani wakishindwa kuzingatia Haki za watumishi taaluma yetu itapuuzwa”
Pamoja na hayo Dokta Nchimbi amekemea vitendo vya rushwa katika kushughulikia masuala ya watumishi badala yake watende haki Kwa Watu wote kwa kufuata Sheria za utumishi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho Gerald Uzika amesema Hadi sasa chama kina Wanachama zaidi ya mia tatu huyo ni moja ya mafanikio makubwa ambayo wameyapata tangu kuanzishwa kwake huku Monica Andrew ambaye ni Naibu Katibu Mkuu THRAPA pamoja na Magreth Haule wakaeleza kupitia maagizo hayo yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM Taifa yataenda kupunguza malalamiko ya Watumishi.