Jeshi la Uganda limetangaza kuwa, limemkamata kamanda wa kundi la waasi la ADF linaloshirikiana na kundi la dola la kiislamu, ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza mabomu yaliyotumiwa na kundi hilo kutekeleza mashambulizi mabaya.
Kamanda huyo Anywari Al-Iraq ambaye ni raia wa Uganda, alikamatwa katika maeneo ya jangwani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako kundi la ADF linaendesha harakati zake.
Katika operesheni ya kumsaka kamnda huyo, watu tisa wakiwemo watoto waliokolewa kutoka katika eneo hilo lililopo mkoani Ituri Mashariki mwa DRC, bidhaa nyengine za kutengenezea mabomu pia zilipatikana huko.
Waasi wa ADF wamekuwa wakiendesha harakati zao kwenye misitu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo kwa zaidi ya miongo miwili sasa, na wamekuwa wakifanya mashambulizi ndani ya nchi hiyo na wakati mwingine ndani ya ardhi ya Uganda.