Washiriki wasiopungua 500 wanatarajiwa kuhudhuria Wiki ya AZAKi 2024 inayosubiriwa kwa hamu na ambayo itafanyikakuanzia Septemba 9 hadi 13 katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Bw Justice Rutenge, alisema tukio hilo la wiki moja ni muhimu kwa maendeleo nchini Tanzania kwa kuwa linawaleta pamoja wadau wakuu wa asasi za kiraia ili kuimarisha mahusiano na ushirikiano. Lengo kuu ni kuimarisha ushiriki wa asasi za kiraia katika maendeleo ya Tanzania kwa kuunda mahusiano mapya na kuimarisha yaliyopo ili kutatua changamoto kuu za kimaendeleo.
“Lengo letu la Wiki ya AZAki ni kuwa na sauti mbalimbali kutoka asasi za kiraia na washirika kujumuika pamoja na kujadili na kupendekeza njia mbali mbali zitakazoisadia Tanzania kupata maendeleo zaidi. Wiki ya AZAKi 2024 itashirikisha asasi za kiraia, zikiwemo asasi zisizo za kiserikali, watendaji wasio wa kiserikali, taasisi za kidini na wananchi wa kawaida, huku kipaumbele kikiwa ni makundi maalumu kama vijana, wanawake na watu wenye ulemavu,”alisema.
Bw Rutenge alikaribisha ushiriki wa Vodacom Tanzania Foundation kama mshirika mkuu wa Wiki ya AZAKi na kuongeza kuwa ushirikiano wa asasi za kiraia ni muhimu katika kupunguza changamoto za kijamii kwani kila mhusika ana jukumu muhimu katika sekta yake.
Wiki ya AZAKi 2024 itakuwa ni wa sita katika mfululizo mikusanyiko iliofanyika 2018, 2019, 2021, 2022 na 2023 na kaulimbiu ya mwaka huu ni “Sauti, Maono, Thamani”. Wiki ya AZAKi 2024 ni jukwaa la ushirikiano katika sekta muhimu.
Wiki ya AZAKi 2024 itafanyika wakati kuna mabadiliko muhimu ya kimataifa na ya ndani ya nchi. Wakati Watanzania wakijiandaa kushiriki katika chaguzi muhimu, tukio hililinatambua nafasi muhimu ya michakato ya kidemokrasia katika kuunda mustakabali wa taifa. Maandamano ya amani ya hivi karibuni yanasisitiza hitaji linaloongezeka la mabadiliko na ushirikishwaji wa raia na hivyo kukuza sauti ya pamoja na kuongeza ufanisi wa kisiasa.
Pia, wakati dunia inakaribia katikati ya utekelezaji wa Malengo ya Kimkakati ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (SDGs) bila kuwepo mafanikio makubwa, Wiki ya AZAKi 2024 inalenga kutumika kama jukwaa la kufikiria upya, kuzingatia upya na kuongeza juhudi kuelekea maendeleo endelevu. Aidha, uundwaji wa Dira ya 2050 unatoa fursa kwa ushirikiano katika sekta zote ili kuchagiza mwelekeo wa maendeleo wa muda mrefu wa Tanzania. Kwa hiyo, kaulimbiu ya Wiki ya AZAKi 2024 inaongozwa na kanuni za dira, sauti na thamani, ikisisitiza ushirikiano kati ya asasi za kiraia, serikali na sekta binafsi kwa maendeleo na ustawi wa Tanzania.
Bi Prudence Zoe Glorious, Mshauri wa Mikakati wa FCS, alisema kaulimbiu ya Wiki ya AZAKi 2024, “Sauti, Dira, Thamani”, inajikita katika ukweli kwamba licha ya majukumu na mitazamo tyofauti ya wahusika wa maendeleo, wote wana wajibu wa pamoja katika kuleta maendeleo ya nchi na kuwahimiza watendaji kutumia sauti zao. Lengo lingine ni kuzungumza, kusikiliza, kushiriki, kuona mbele na kujadilinjia zinazoweza kuleta thamani halisi na chanya kwa kufikia maono ya pamoja ya mustakabali wa nchi yetu.
● Sauti: Inasisitiza umuhimu wa mitazamo mbalimbali na ushirikishwaji. Inaalika kila Mtanzania, kuanzia wanaharakati wa ngazi za chini hadi viongozi wa kitaifa wa biashara, kuchangia maarifa na uzoefu wao. Inahusu kuhakikisha kwamba sauti ya kila mtu inasikika katika mazungumzo ambayo yanaunda mustakabali wa taifa letu, hasa katika kuelekea uchaguzi muhimu.
● Dira: Pamoja na uundwaji wa Dira ya 2050 kuwa kituo cha kati, kuna haja ya kuoanisha matarajio yetu ya pamoja ya mustakabali wa Tanzania. Ni mwaliko wa kuoanisha juhudi na mikakati yetu ya kujenga mustakabali unaoakisi malengo yetu ya pamoja. “Maono” yatatupa changamoto ya kuweka mielekeo iliyo wazi na ya pamoja ambayo itaongoza matendo yetu sasa na siku zijazo.
● Thamani: Kulenga katika kutoa manufaa yanayoonekana kwa Watanzania, “Thamani” inahusu kufikiria vitendo ambavyo vitaleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya watu kupitia hatua zetu za pamoja. Inawasilisha ahadi yetu kwa matokeo ya vitendo ambayo huinua na kuwezesha kila raia.
“Sauti, Dira, Thamani” ni wito ufaao wa ushirikiano katika sekta zote muhimu za jamii ya Kitanzania—mashirika ya kiraia, serikali, na sekta binafsi—ukisisitiza umuhimu wa michango mbalimbali kuelekea lengo moja: maendeleo na ustawi wa taifa.