Makumi kwa maelfu ya Wairani walimiminika katika mitaa ya Tehran Jumatano ili kujiunga na maandamano kwaajili ya mazishi ya rais Ebrahim Raisi na wasaidizi wake, waliofariki katika ajali ya helikopta siku ya Jumapili.
Katikati ya mji huo, watu waliokuwa na picha za Raisi walikusanyika ndani na karibu na Chuo Kikuu cha Tehran, ambapo Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei anatarajiwa kuongoza sala kwa ajili ya Raisi na masahaba zake, akiwemo waziri wa mambo ya nje Hossein Amir-Abdollahian.
Helikopta ya Raisi ilianguka Jumapili kwenye ukingo wa mlima uliofunikwa na ukungu kaskazini mwa Iran ikiwa njiani kuelekea mji wa Tabriz baada ya kundi hilo kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa bwawa kwenye mpaka na Azerbaijan.
Operesheni kubwa ya utafutaji na uokoaji ilizinduliwa, ikihusisha msaada kutoka Turkiye, Urusi na Umoja wa Ulaya. Televisheni ya serikali ilitangaza kifo cha Raisi mapema Jumatatu.
Raisi, ambaye alitarajiwa sana kumrithi Khamenei kama kiongozi mkuu, alikuwa na umri wa miaka 63.
Katika mji mkuu, mabango makubwa yamepandishwa yakimsifu rais aliyefariki kama “mfia imani,” huku mengine yakiaga “mtumishi wa watu wasiojiweza.”