Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema atavunja Mabaraza ya Madiwani yenye mivutano inayokwamisha maendeleo ya Wananchi.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo wakati wa kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya inayojengwa Kata ya Kibelege katika Halmashauri ya Mji Ifakara na kubaini kuwa imeshindwa kukamilika kutokana na mivutano ya kisiasa uliotokea mara tu fedha za ujenzi wa Hospitali hiyo zilipofika.
Amesema mivutano ya kisiasa ya Madiwani husababisha miradi mbalimbali ya maendeleo kusimama na kutokamilika kwa wakati na kusisitiza kuwa
atachukua hatua mara moja ikiwa ni pamoja na kuvunja Baraza la Madiwani la Halmashauri husika.
Mchengerwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza Watendaji katika Halmashauri Nchi nzima kuacha mivutano na Wanasiasa na kusababisha ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo.