Zimbabwe imezuia mali mbili zinazomilikiwa na bosi wa Msalaba Mwekundu wa Uganda, Robert Kwesiga, na mkewe kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu, ripoti ya vyombo vya habari nchini Zimbabwe ikinukuu mamlaka ya mashtaka nchini humo.
Thamani ya nyumba hizo mbili, inayokadiriwa kufikia dola 300,000, hailingani na mapato ya Kwesiga wakati wa kuajiriwa kwake na Shirika la Msalaba Mwekundu la Denmark nchini Zimbabwe kati ya 2007 na 2013, gazeti linalodhibitiwa na serikali la Herald likinukuu taarifa ya mamlaka hiyo.
Mahakama kuu ilitoa amri ya kusitishwa kwa muda wiki jana kufuatia ombi la ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu.
“Aidha, wao au mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba yao anazuiwa kutoa mali hiyo hadi pale amri itakapobadilishwa au kutenguliwa na mahakama,” ilisema mamlaka hiyo katika taarifa yake.