WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wafuatilie mienendo ya watoto wao waendapo shuleni ikiwemo na mahudhurio na masomo yao darasani.
“Serikali inaendelea kuimarisha mahudhurio ya watoto shuleni kwa kuzungumza na wazazi ili kuhakikisha kila mzazi anasimamia mahudhurio ya mtoto wake, kwenda shule, kuingia darasani, lakini anaporudi nyumbani, mzazi afuatilie mwenendo wa masomo ya mtoto huyo ili ajiridhishe kama kweli mtoto alikwenda shuleni.”
Ametoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Mei 23, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alihoji Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanafunzi wanaoanza masomo wanamaliza wote shule ukiacha wale ambao hufariki dunia.
Katika ngazi ya shule za sekondari, Waziri Mkuu amesema: “Tunaimarisha ujenzi wa mabweni na hosteli kwaajili ya wanafunzi wa kike na wa kiume ili wasome palepale, walale pale, wacheze pale lakini pia usimamizi wa maadili yao uweze kuimarika.”
Amesema maelekezo yalikwishatolewa kwenye Halmashauri zote za Wilaya kwani ndizo zinasimamia shule za msingi na sekondari na kwenye ngazi za mikoa ili wafanye ufuatiliaji shuleni. “Pia tumeimarisha taasisi yetu ya Uthibiti Ubora ambayo moja ya majukumu yake ni kuhoji idadi ya wanafunzi waliosajiliwa, waliopo darasani na wanatakiwa wahoji ni kwa nini wengine hawapo kulingana na usajili uliopo.”
“Tunaamini kupitia hatua hizi, utoro utapungua na tutaanza kuona wanafunzi waliosajiliwa wanafikia asilimia 95 hadi 98 ya wanaomaliza.”