Mahakama ya Tunisia Jumatano iliwahukumu wanahabari wawili wa televisheni na redio kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kuikosoa serikali kwenye vipindi vyao na kwenye mitandao ya kijamii.
Borhane Bsaïs na Mourad Zeghidi walipewa kila mmoja kifungo cha miezi sita kwa kusambaza “habari za uwongo” na miezi sita ya ziada kwa “kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kuwachafua wengine,” akimaanisha Rais wa Tunisia Kaïs Saied, msemaji wa mahakama Mohamed Zitouna alisema.
Hukumu hizo zinakuja chini ya wiki mbili baada ya wote kukamatwa. Wao ni miongoni mwa kundi pana la wanahabari, wanaharakati na wanasheria walioshtakiwa chini ya Amri ya 54, sheria inayoharamisha usambazaji wa “habari bandia” zinazolenga kudhuru usalama wa umma au ulinzi wa taifa.
Sheria hiyo iliyopitishwa mwaka 2022 kupambana na uhalifu wa mtandaoni, imekosolewa vikali na watetezi wa haki za binadamu wanaosema makosa hayo yamebainishwa wazi na yanatumika kuwakandamiza wakosoaji wa rais.
Bsaïs na Zeghidi wote walikanusha madai hayo.
Mahakamani, walirejelea sheria zinazolinda uhuru wa kujieleza ambazo Tunisia iliziweka baada ya mapinduzi yake ya 2011, wakati ilipokuwa nchi ya kwanza Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kumuangusha dikteta wa muda mrefu. Wote wawili walisema walikuwa wakifanya kazi zao tu, kuchambua na kutoa maoni kuhusu maendeleo ya kisiasa na kiuchumi nchini Tunisia.