Bodi ya bima ya amana imesema inaendelea na ufilisi wa benki takribani saba zilizofungwa na benki kuu ya Tanzania mwaka 2018 ambapo Joyce Shala ambaye ni afisa mwandamizi wa bodi amesema kwa sasa wamekamilisha sehemu ya ufilisi kwa sehemu kubwa na wananchi wanaendelea kupata stahiki zao kwa mujibu wa sheria.
Ameeleza hayo mkoani Njombe wakati akizungumza na wadau mbalimbali wakiwemo watendaji katika halmashauri ya mji wa Njombe,Makambako pamoja na halmashauri ya wilaya ya Njombe kwa lengo la kutoa elimu juu ya uwepo wa bima ya amana na fidia ya bima ya amana ambayo kwa sasa imeongezeka mpaka kufikia ukomo wa shilingi milioni saba na laki tano.
“Bodi ya bima ya amana inaendelea na ufilisi wa benki takribani saba na tumeshakamilisha sehemu ya ufilisi kwa sehemu kubwa na wananchi wanapata stahiki zao kwa mujibu wa sheria,lengo la kuja hapa Njombe ni kwasababu ya iliyokuwa benki ya NJOCOBA ambayo ilifungwa mwaka 2018 ambapo kwa kipindi hicho fidia ya bima ya amana ilikuwa kuanzia shilingi moja mpaka mpaka milioni moja na laki tano,kwa hiyo kwa wateja wa benki ya NJOCOBA wamefanikiwa kupata stahiki kwa asilimia mia moja”amesema Joyce
Vilevile ametoa wito kwa wananchi wote waliokuwa wateja kwa iliyokuwa benki ya NJOCOBA ambao hawajaweza kuchukua fidia ya bima ya amana kufika katika benki ya TCB wakiwa na vitambulisho vyao ili kufanyiwa uhakiki na kupata stahiki zao.
“Benki ya NJOCOBA ilikuwa na wateja takribani elfu 12,323 na ambao wameshachukua pesa zao mpaka sasa ni wateja 4,014 huku kiasi ambacho kimelipwa mpaka sasa ni Bilioni 1.2 sawa na 87% ya madai ya wateja na ambao hawajachukua bima ya amana ni takribani wateja 8,309 na kiasi wanachodai ni Milioni 189 kwa hiyo hawa ndio tunawahimiza waweze kuchukua fedha zao lakini pia kuna watu ambao wanadaiwa ambapo tunadai zaidi ya milioni 431″aliongeza Joyce
Erasto Mpete ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe na mwenyekiti wa kamati ya madai wa iliyokuwa benki ya NJOCOBA amesema bima ya amana imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha wateja wengi waliokuwa wakiidai benki hiyo wamekwisharejeshewa fedha zao na kutoa wito kwa wachache waliobaki kutumia fursa iliyopo ili kwenda kuchukua fedha zao.