Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza rasmi tarehe za maadhimisho ya Kumbukizi ya Hayati Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa awamu ya tatu na msarifu mwanzilishi wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation.
Kumbukizi hii inategemewa kufanyika tarehe 29-31 Julai, 2024, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwl. Julius Nyerere (JNICC), Dar Es Salaam. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anategemewa kuwa mgeni rasmi wa Kumbukizi hii siku ya kilele cha maadhimisho haya tarehe 31 Julai 2024.
Kauli mbiu ya Kumbukizi ya mwaka huu ni “Kuchagiza Uendelevu wa Ndani kuelekea kwenye Upeo Mpya” (Mkapa’s Legacy: Taking local sustainability to new horizons”).
Kauli mbiu hii inaangazia maono na kazi mbalimbali za Hayati Benjamin Mkapa katika kuongeza chachu ya maendeleo ya ndani ya nchi, kwa kutumia raslimali, sera na mifumo ya ndani katika kuleta maendeleo. Maono haya aliyaishi Mheshimiwa Mkapa, akiamini kuwa Afrika yote ina uwezo wa kujiletea maendeleo yake yenyewe kwa kuzingatia vyanzo na rasilimali zake za ndani, ikichagizwa na mashirikiano na marafiki wa maendeleo wa ndani na nje ya Afrika.
Wageni wanaotarajiwa kushiriki kilele cha Maadhimisho haya tarehe 31 Julai 2024, ni pamoja na Mheshimwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza (ambaye pia ni msarifu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation),Familia ya Mheshimiwa Mkapa, Viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi, marafiki wa Mheshimiwa Mkapa wa ndani na nje ya nchi, Wawakilishi wa Asasi zisizo za Kiserikali, Wadau wa Maendeleo, Viongozi wa Dini, Wataalamu wa Afya wa sekta mbalimbali, Wananchi Mashuhuri, Waandishi wa Habari n.k.
Mwaka huu, kumbukizi hii itaanza kwa majadiliano ya kitaifa ya kitaalamu ya siku mbili juu ya masuala ya rasilimali watu katika sekta ya afya, yaliyopewa jina la “National Human Resource for Health (HRH) Conference”. Majadiliano haya yatafanyika Julai 29-30, 2024 kuelekea kilele cha Kumbukizi kitakachoadhimishwa Julai 31,2024.
Kwa upande wa mkutano wa kitaalamu yaani “National Human Resources for Health Conference”, suala la rasilimali watu katika sekta ya afya ndio linalobeba dhima ya mkutano.
Kwa sasa Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi zinazohusiana na watumishi wa afya ikiwemo pia upungufu wa takribani asilimia 66 ya watumishi wa afya katika vituo vya kutolea huduma za afya. Kukabiliana na hizi changamoto hatuna budi kuunga mkono jitihada za Serikali tukiwa kama wadau wa sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutatuamapungufu hayo.
Aidha Mkutano huu utawaleta wadau mbalimbali kutoka Serikali, Wadau wa maendeleo, sekta binafsi, Vyuo Vikuu, wataalamu wa sekta ya afya, pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali. Lengo kuu ni kubadilishana uzoefu, maarifa, kubaini fursa za masomo na ajira za ndani na nje ya nchi kwa wataalam wa afya, na pia kupendekeza mikakati ya pamoja ya kupunguza changamoto za raslimali watu katika sekta ya afya nchini.
Kumbukizi hii ya Hayati Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ni ya tatu kufanyika tangu kufariki kwake 23 Julai, 2020.
Kumbukizi ya kwanza ilifanyika Julai 2021 jijini Dar es Salaam, na ya pili ilifanyika Julai 2022, Zanzibar. Aidha Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation iliamua kufanyika kwa kumbukizi hii kila baada ya mwaka mmoja, na hivyo kupelekea kumbukizi ya tatu kufanyika Julai, 2024.