Balozi wa Marekeni nchini Tanzania, Mhe. Michael A. Battle Snr, amezindua Kampeni ya GGM Kili Challenge 2024 katika hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuchangisha fedha kwa lengo la kukusanya Dola za Kimarekani milioni 1 kusaidia jitihada za serikali ya Tanzania katika kupambana na UKIMWI.
Ahadi za michango zinatarajiwa kukamilishwa ifikapo katikati ya Julai 2024. Kilimanjaro Challenge ya Geita Gold Mining Limited (GGML) dhidi ya UKIMWI, iliyoanzishwa mwaka 2002, ni shirika la ushirikiano wa hisani linaloleta pamoja serikali kupitia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na GGML ili kuchangisha fedha na kuhamasisha juhudi za kupambana na ugonjwa huo nchini.
Moja ya shughuli zinazojulikana zaidi za kuchangisha fedha kwa ajili ya kusudi hili ni Kili Challenge, ambayo inahusisha kupanda na kuzunguka Mlima Kilimanjaro kila mwaka. Washiriki hununua tiketi za Challenge kama sehemu ya kampeni yao ya kuchangisha fedha.
Wakati baadhi ya ada inagharamia kupanda mlima na kuendesha baiskeli, sehemu kubwa ya fedha inaingia kwenye Kili Trust Fund, na hutumika kusaidia mapambano ya kitaifa dhidi ya UKIMWI. Mfuko wa Kili ni mchangiaji mkuu wa Mfuko wa Taifa wa UKIMWI.
Katika mwaka wake wa 22, kampeni inaanza tarehe 19 Julai na itahitimishwa tarehe 25 Julai 2024.
Akizungumza katika Hoteli ya Hyatt wakati wa uzinduzi, Balozi wa Marekani alisifu GGML na TACAIDS kwa kushirikiana kwenye kampeni kama hii inayosaidia serikali kupambana na kuenea kwa UKIMWI nchini.
“Jitihada hii inapaswa kupongezwa na nina himiza wadau zaidi kusaidia kupambana na janga hili (UKIMWI),” alisema Balozi wa Marekani. Duan Archery, Mkurugenzi Mtendaji wa Geita Gold Mining Limited (GGML), alieleza furaha yake kwamba makampuni mengi yamehudhuria hafla ya kuchangisha fedha hapa Dar es Salaam.
“Michango yenu ni ya thamani kubwa na itatusaidia kufikia lengo letu la ‘kufikia sifuri’,” alitanabaisha.
Malengo matatu ya sifuri ni kutokuwepo kwa maambukizi mapya, kutokuwepo kwa ubaguzi, na kutokuwepo kwa vifo vinavyohusiana na UKIMWI. Kwa mujibu wa Archery, mwaka huu GGML inasaidia washiriki 60: wapandaji mlima 42 na waendesha baiskeli 18.
Wawili kati ya washiriki hawa ni watoto wadogo, mvulana na msichana kutoka Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma cha Geita, ambacho kilianzishwa mwaka 2006 kwa ufadhili kutoka Kilimanjaro Challenge.
Simon Shayo, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti wa Masuala ya Uendelevu na Mambo ya Ubia (Afrika) alisema vikundi mbalimbali vimefaidika na kampeni hiyo, ikiwa ni pamoja na watoto wa Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma, ambacho pia kinawatunza watoto wengine walio katika mazingira magumu.
“Kundi la kwanza la watoto waliokulia katika kituo hicho sasa wanasoma vyuoni, wakiwemo wawili wanaosoma digrii za udaktari,” alibainisha Shayo. Wakati huo huo, Dkt. Jerome Kamwela, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, alisema kuwa fedha zote zitakazokusanywa zinagawanywa kwa mashirika yanayohusiana na UKIMWI.
Kwa mujibu wake, vita dhidi ya UKIMWI inahitaji msaada zaidi wa ndani, hasa wakati michango ya kigeni inapopungua.