Shirika la uangalizi wa vyombo vya habari la Reporters Without Borders (RSF) lilisema Jumatatu liliwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuhusu waandishi wa habari wa Kipalestina waliouawa au kujeruhiwa huko Gaza.
RSF ilisema inamwomba mwendesha mashtaka wa ICC kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa na jeshi la Israel dhidi ya angalau waandishi tisa wa Kipalestina tangu Desemba 15.
Mahakama ya ICC ilisema mwezi Januari ilikuwa inachunguza uhalifu dhidi ya waandishi wa habari tangu kuzuka kwa vita kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas huko Gaza, ambayo imegharimu maisha ya zaidi ya waandishi 100.
RSF ilisema ilikuwa na “sababu nzuri za kufikiri kwamba baadhi ya waandishi wa habari hawa waliuawa kimakusudi na kwamba wengine walikuwa waathirika wa mashambulizi ya makusudi ya IDF (Jeshi la Ulinzi la Israel) dhidi ya raia.”
Malalamiko haya mahususi — ya tatu ambayo RSF imetoa — yanahusu waandishi wanane wa Kipalestina waliouawa kati ya Desemba 20 na Mei 20, na mwingine mmoja ambaye alipata majeraha.