Mwanariadha nyota wa Kenya, Beatrice Chebet ameweka rekodi ya dunia mbio za mita 10,000 baada ya kushinda Eugene Diamond League nchini Amerika kwa dakika 28:54.14, Jumamosi.
Alifuta rekodi ya raia wa Ethiopia Letesenbet Gidey aliyetimka umbali huo kwa dakika 29:01.03 mjini Hengelo, Uholanzi mnamo Juni 8, 2021.
Chebet, ambaye ni bingwa wa mbio za nyika duniani, ameimarisha muda wake bora kutoka dakika 33:29 aliotimka Machi 2020 ugani Kasarani jijini Nairobi hadi 28:54.14.
Alifuatwa kwa karibu na raia wa Ethiopia Gudaf Tsegay (29:05.92) na Wakenya Lilian Kasait (29:26.89) na Margaret Chelimo (29:27.59) ambao walipata muda bora kila mmoja.
Bingwa huyo wa mbio za mita 5,000 za Jumuiya ya Madola na Afrika, ambaye pia ni mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita tano barabarani, pia amefuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa mnamo Julai 26 hadi Agosti 14. Mbio hizo zilivutia washiriki 21 wakiwemo Wakenya 15.