Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kujenga hoteli ya nyota tano mkoani Katavi ikiwa ni muendelezo wa uboreshaji miundombinu mbalimbali katika sekta ya utalii ikiwemo huduma za malazi ili kukidhi mahitaji kutokana na ongezeko la idadi ya watalii Nchini.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) wakati akijibu swali la Mhe. Sebastian Simon Kapufi (Mb) aliyetaka kujua ni lini ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano ya Ujenzi wa hoteli ya nyota tano katika Mji wa Mpanda itaanza kutekelezwa.
Aidha Mhe. Kitandula alisema kuwa TANAPA imepata eneo lenye ukubwa wa hekta 15.37 lililopo Kitalu A (Kiwanja Na. 12) katika eneo la Magamba-Mpanda Mjini kwa ajili ya ujenzi wa hoteli hiyo ya nyota tano, na kwamba tayari hati ya eneo hilo imepatikana. Vilevile ilielezwa kuwa ili kulinda eneo hilo, tayari TANAPA imechonga barabara pembezoni mwa eneo husika.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa shughuli za uendelezaji wa eneo hilo umechukua muda kutokana na ufinyu wa bajeti. Hata hivyo, kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kufanya upembuzi yakinifu kuhusu Mradi huo kabla ya kuanza utekelezaji wake.
”Wizara ya Malisili na Utalii baada ya kukamilisha ujenzi wa hoteli hiyo inatarajia kushirikisha sekta binafsi kwa ajili ya kuendesha biashara hiyo ili kujenga imani na kuvutia wawekezaji wengine kuwekeza katika sekta ya Utalii mkoani Katavi”
Mhe. Kitandula alitumia fursa hiyo kuupongeza mkoa wa Katavi kwa kuandaa mkakati wa utalii na kubainisha vivutio vya utalii vilivyopo Katavi. Aidha alisema wizara inaoanisha yaliomo katika mkakati huo katika mipango ya wizara kwa ajili ya kuvitangaza vivutio vinavyopatikana Nchini Tanzania.