Sasa ni rasmi kwamba meneja wa zamani wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani Hansi Flick ndiye anachukua mikoba ya kuinoa Barcelona.
Miamba hao wa Uhispania walitangaza uteuzi wa Flick siku ya Jumatano, siku chache tu baada ya kuondoka kwa Xavi.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 sasa ataisimamia Barca hadi Juni 2026 baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo.
“FC Barcelona na Hansi Flick wamefikia makubaliano kwa Mjerumani huyo kuwa kocha wa timu ya kwanza ya soka ya wanaume hadi 30 Juni 2026. Kocha mpya ametia saini mkataba katika ofisi za Klabu akifuatana na rais wa FC Barcelona Joan Laporta; makamu wa kwanza wa rais anayehusika na eneo la michezo, Rafa Yuste na mkurugenzi wa michezo wa Klabu, Anderson Luís de Souza, Deco,” Barcelona ilisema katika taarifa Jumatano.
Flick, ambaye alitimuliwa na Ujerumani mnamo Septemba 2023, anachukua nafasi ya Xavi, ambaye alitimuliwa wiki iliyopita.