Wananchi Iwungilo waondolewa hofu juu ya fedha ya ujenzi wa kituo cha afya kulipwa mwenyekiti
Wananchi wa kijiji cha Iwungilo halmashauri ya mji wa Njombe wameondolewa hofu juu ya fedha yao takribani shilingi milioni kumi na tisa ya ujenzi wa kituo cha afya kulipwa kijiji huku akihusishwa mwenyekiti wa kijiji hicho bwana Joseph Myamba na kuzua taharuki kwa wananchi kutokana na taarifa iliyotolewa na Daktari ambaye ni msimamizi wa ujenzi wa kituo cha afya cha kata hiyo.
Akizungumza baada ya mkutano na wananchi uliokuwa na lengo la kutoa ufafanuzi juu ya fedha hiyo,mwenyekiti wa kijiji bwana Myamba amesema kuwa wamefanya mkutano huo kutokana na taharuki iliyotokea katika mkutano wa mwezi wa tatu ambapo taarifa ya daktari ilieleza kuwa kiasi hicho cha fedha kimelipwa kwa kijiji huku mwenyekiti akihusishwa kwa kuwa alikuwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kituo hicho cha afya.
“Taarifa za mganga alizitoa kuwa Milioni kumi na tisa zimelipwa kwenye kijiji haikumaanisha kuwa kijiji ndio kimelipwa ile fedha,kwenye matamshi ilitamkwa vibaya isipokuwa ile hela ililipwa material yaliyoweza kufanya kazi kwenye kituo cha afya kwa hiyo baada ya mkutano huu umezaa matunda kwa kuwa wananchi walidhani labda ile hela iliingia kwa matumizi binafsi lakini ni hela ambayo ilifanya kazi ya matumizi ya kituo cha afya kwa hiyo wananchi wameelewa na wameridhia kuona mradi unaendelea vizuri”amesema Myamba
Akitoa ufafanuzi juu ya fedha hiyo mtendaji wa kata ya Iwungilo Bonasius Mwalongo amesema amekaa na wenyeviti wa vitongoji ili kujua michango yao na kubaini kiasi cha milioni nne na elfu kumi na tano ambayo ndio iliyotumika utoka kwenye kijiji kwa ajili ya ujenzi.
“Kila kitongoji material yake aliyoyaandaa yakaenda kituo cha afya jumla yake ndio hayo yenye thamani ya milioni nne na elfu kumi na tano nikahoji mbona zinatajwa milioni kumi na tisa lakini kuna wananchi wa hapa na wengine sio wa hapa walipeleka mawe nao wakajumuishwa kwenye hiyo milioni kumi na tisa ambao walilipwa hela hiyo kwa hiyo wote waliolipwa wamekiri”amesema Mtendaji Mwalongo wakati akitoa ufafanuzi
Awali wananchi wa kijiji hicho wamesema uongozi ulipaswa kutoa ufafanuzi wa kueleweka ili kuondosha sintofahamu hiyo kwasababu ilileta shida kupata taarifa kuwa mwenyekiti amepokea kiasi cha milioni kumi na tisa ya malipo kutoka kwa mganga.