Maafisa Rasilimali Watu Wanalo jukumu la kumuunganisha mwajiri na waajiriwa ili kuhakikisha haki na maslahi yao yanatekelezwa katika kulinda nguvu kazi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, wakati akifungua Kikao Kazi kilichofanyika mjini Kibaha, cha kuwajengea uwezo Maafisa Rasilimali Watu na Maafisa Usalama na Afya mahali pa Kazi, jinsi ya kutambua vihatarishi na huduma zinazotolewa na WCF, na hatua za kufuata wakati wa kuwasilisha madai ya fidia kwa wafanyakazi, hususan kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao.
Aidha Dkt. Mduma alisema, kwa upande wa Maafisa wanaosimamia Usalama na Afya mahali pa Kazi, wao wanaowajibu wa kuwaunganisha wafanyakazi na mwajiri ili usalama na afya mahali pa kazi vinapewa kipaumbele na kuhakikisha kanuni zinazingatiwa kikamilifu.
“Ni wajibu wa mwajiri kujisajili na kumchangia mwajiriwa katika Mfuko ili anapopatwa na changamoto ya ajali au ugonwja unaotokana na kazi, WCF iweze kumlipa fidia.” Amefafanua Dkt. Mduma na kuongeza..
“Mtafahamu na ni bayana kwamba azma ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasssan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na uchumi endelevu. kwa ile dhana pana ya maana ya uchumi edelevu ni uchumi usiemwache mfanyakazi nyuma, hata anapopatwa na madhila anapotekeleza wajibu wake kwa mwajiri wake,” alibainisha
Alisema, endapo ikitokea mwajiriwa amepatwa na madhila ya ajali au magonjwa yanayotokana na kazi, hii itamuyumbisha katika utaratibu wake wa maisha na hapo ndipo WCF inafanya jukumu lake kuanzia kutoa matibabu kwa wakati, kufidia ulemavu uliojitokeza au kulipa fidia kwa wategemezi pale inapotokea mfanyakazi amepoteza maisha,” alifafanua.
Awali Mkurugenzi wa Hududma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar, alisema mafunzo kama hayo pia yamekuwa yakitolewa kwa madaktari kwa lengo la kuwawezesha kupata uelewa wa kutosha kuhusu shughuli zinazotekelezwa na WCF na hivyo kusaidia utekelezaji wa kulipa fidia kwa mujibu wa sheria.