Balozi wa Tanzania nchini Korea (Jamhuri ya Korea), Mhe Balozi Togolani Mavura amekanusha taarifa iliyosambazwa na chombo kimoja cha habari kuwa Tanzania imepokea mkopo toka Jamhuri ya Korea na kutoa sehemu ya bahari na madini.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X (zamani Twitter), Balozi Togolani ameandika,
“Taarifa hii ina mapungufu makubwa ya kiuandishi, kiuweledi na haiakisi ukweli kwa sababu:
1. Tanzania haijasaini Mkataba wowote na Jamhuri ya Korea unaohusu Bahari wala Madini katika ziara ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu nchini Korea. Katika ziara hiyo, Rais ameshuhudia utiwaji saini wa Mkataba MMOJA tu ambao ni mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.
Mbali na mkataba huo, Mheshimiwa Rais alishuhudia utiwaji saini wa Hati ya Maelewano (Memorandum of Understanding-MOU) mbili za Ushirikiano katika sekta za Uchumi wa Bluu na Madini ya Kimkakati. Aidha, alishuhudia pia kusainiwa kwa Tamko la Utayari wa Kuanza Majadiliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (Joint Statement on the launch of Negotiation on Economic Partnership Agreement-EPA).
Hivyo, Tanzania na Korea wametiliana saini Mkataba mmoja; MOUs mbili, na Tamko moja.
2. Tanzania haijagawa chochote kubadilishana na mkopo nafuu kutoka Korea kama ilivyoandika.
Tanzania inapata mkopo wa masharti nafuu kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo (EDCF) kwa mara ya tatu. Mara ya kwanza dola za kimarekani milioni 733 (2014-2020); mara ya pili dola bilioni 1 (2021-2025) na huu mkopo wa tatu ni dola bilioni 2.5 (2024-2028).
Nchi 59 zilizoko barani Afrika, Asia na Ulaya zinafaidika na mkopo wa aina hii kutoka EDCF edcfkorea.go.kr/he/HPHYFE043M01
3. Tofauti na mlivyoandika, mkopo huu wa masharti nafuu una riba ya asilimia 0.01, unalipwa kwa miaka 40, na una fungate (grace period) ya miaka 25. Yaani unaanza kulipa baada ya mwaka wa 26. Hivyo si kweli kwamba mkopo huo utalipwa kwa miaka 5.
Ni mategemeo yangu kuwa mtakuwa na uungwana wa kurekebisha taarifa hii.”