Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na shirika la HelpAge Tanzania kwa fahari imeungana na jamii ya kimataifa katika kuadhimisha kwa mara ya Kwanza siku ya kimataifa ya Teknolojia Saidizi tarehe 4 Juni 2024.
Tukio hili muhimu ni sehemu ya kampeni ya “Fungua Kila Siku”, ambayo inalenga kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa teknolojia Saidizi na hitaji la haraka la kuboresha upatikanaji wake, hususan katika nchi za kipato cha chini na kati
Siku ya kimataifa ya Teknolojia Saidizi ni mpango wa pamoja uliozinduliwa na mashirika yanayoongoza katika afya na maendeleo kukuza ujumuishaji.
Akiongea mbele ya waandishi wa habari Rasheed H.Maftah mkurugenzi kitengo cha watu wenye ulemavu,ofisi ya waziri mkuu-kazi vijana ,ajira na wenye ulemavu amesema Kampeni ya “Fungua Kila Siku” ilizinduliwa rasmi huko Davos, Uswisi, wakati wa Jukwaa la Uchumi Duniani tarehe 16 Januari 2024.
Tekinolojia Saidizizi inajumuisha bidhaa, mifumo, na huduma zinazoongeza utendaji na uhuru wa mtu katika maeneo kama vile utambuzi, mawasiliano, kusikia, uhamaji, kujitunza, na kuona.
Teknolojia hizi ni muhimu katika kuwezesha afya, ustawi, ujumuishaji, na ushiriki katika shughuli za kijamii na za kijamii.
Mifano ya Tekinolojia Saidizi ni pamoja na bidhaa za kimwili kama viti vya magurudumu, miwani, viungo bandia, fimbo nyeupe, na vifaa vyakusaidia kusikia, pamoja na suluhisho za kidijitali kama programu za utambuzi wa sauti na huduma za maandishi ya maneno.
Naye Smart Daniel Mkurugenzi mtendaji HelpAge Tanzania amesema kuwa duniani kote, takribani, watu bilioni 2.5 wanahitaji bidhaa moja au zaidi ya tekinolojia saidizi, lakini ni asilimia 10 tu ya watu katika nchi za kipato cha chini wanaweza kupata Tekinolojia Saidizi wanayohitaji, ikilinganishwa na asilimia 90 katika nchi za kipato cha juu.
‘Hapa Tanzania, data za kitaifa zinaonyesha kuwa asilimia 11.2 ya idadi ya watu wana hali ya ulemavu hivyo upatikanaji wa Tekinolojia Saidizi nchini Tanzania mara nyingi ni wa dharura na unategemea misaada, hali hii haitoshi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya idadi ya watu wanaozeeka, wenye ulemavu na kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs)’.
Upo umuhimu wa Kuboresha Upatikanaji wa Tekinolojia saidizi kwani kuboresha upatikanaji wa Tekinolojia Saidizi ni muhimu kwa kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeachwa nyuma.
Tekinolojia Saidizi ni haki muhimu ya binadamu katika kutengeneza usawa na kuwezesha kila mtu kuishi maisha yenye kuridhisha.