Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuuangalia upya utaratibu wa walimu wa shule za msingi kuwa na utaratibu unaofanana wa kuingia na kutoka kazini kwa mazingira ya mjini na vijijini.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa maelekezo hayo bungeni jijini Dodoma wakati wa maswali kwa Waziri mkuu alipokuwa akijibu swali la Mariam Kisangi mbunge wa Viti maalum aliyehoji mwongozo wa serikali unaowafanya watumishi wa kada moja kutofautiana muda wa kutoka kazini hasa walimu wa shule za msingi ambao kwa shule za mjini hutoka saa 08:30 na vijijini hutoka saa 10:30.
Akijibu swali hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema “kinachopelekea tofauti ya muda wa kutoka ni mazingira ya maeneo hayo ya mijini na vijijini kwa maeneo ya mijini kwa mara nyingi ofisi za elimu na kwakupata kibali kutoka TAMISEMI wanafunzi na walimu wakiingia asubuhi hawapati muda wa kupumzika na hivyo wanaunganisha hadi saa 08:30 lakini vijijini muda wa mchana wanapata nafasi ya kurudi nyumbani Kwenda kula kwahiyo muda wa kula unakwenda kulipiwa pale mbele na kufanya muda wa kutoka kuwa mrefu zaidi lakini masaa ya kazi ni yale yale na huu ni mpango kazi uliowekwa kulingana na mazingira yaliyopo”
Katika kusisitiza hilo ameiomba Ofisi ya Rais Tagala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuupitia upya muongozo huo ili kuweka usawa wa watumishi hao.