Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) itaanza kununua mazao ya wakulima kuanzia Julai 15 hadi 20 mwaka huu katika vituo vya ununuzi ambavyo vitatangazwa hapo baadae.
Mhe Bashe ameyasema hayo tarehe 5 Juni, 2024 jijini Dodoma katika Hafla ya Utiaji Saini Randama za Mashirikiano kati ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania ( CPB), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) iliyohusisha makubaliano ya mauziano ya tani 60,000 za mahindi meupe kati ya CPB na WFP yenye thamani ya Dola za Marekani 22,000.
Waziri Bashe amesema Serikali itaendelea kutafuta masoko ya uhakika na kutarajia kusaini mikataba mingine ya mauziano ya mazao na Shirika la WFP ambalo limekuwa na mchango endelevu katika kutoa fursa za masoko ya moja kwa moja kwa wakulima wadogo wa mazao ya mahindi, mtama, maharage na mazao mengineyo katika kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini.
Viongozi waliohudhuria ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo akiwemo Makamu Mwenyekiti, Bi. Mariam Ditopile (Mb).