Wazalishaij wa vyakula vya mifugo nchini wametakiwa kuwasilisha sampuli za vyakula hivyo katika Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kwa mujibu wa sheria ili kuhakiki ubora wa vyakula hivyo kabla ya kupelekwa sokoni.
Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo (08.06.2024) ofisini kwake jijini Dar es Salaam mara baada ya timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na TVLA kukamilisha ukaguzi wa baadhi ya viwanda vya vyakula hivyo na kufanya kikao cha utoaji mafunzo kwa wazalisha, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana na umuhimu wa uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo juni 6 Mkoani Arusha.
Dkt. Bitanyi ameongeza kuwa wazalishaji hao wanapaswa kuwasilisha sampuli katika maabara za wakala hiyo ili wapatiwe ushauri wa vyakula hivyo na sheria inataka chakula kisicho bora kisingizwe sokoni ili kumlinda mfugaji.
“Wazalishaji wa vyakula vya mifugo wahakikishe wanaendelea kuzalisha vyakula bora ili wafugaji waweze kukinunua chakula hicho, ili aweze kupata matokeo mazuri kwa mifugo yake.” Amesema Dkt. Bitanyi
Akiongoza timu ya ukaguzi, Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka TVLA Dkt. Zacharia Makondo, amesema ni muhimu kwa vyakula vya mifugo kufika sokoni kama vilivyowekwa viwandani na kwamba wanaopuuza suala la kupima na kuhuisha usajili wa viwanda vyao watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama.
Akizungumza jijini Arusha kwenye kikao cha utoaji mafunzo kwa baadhi ya wazalisha, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya mifugo kuhusiana na umuhimu wa uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Dkt. Makondo amefafanua kuwa katika ukaguzi wamegundua baadhi ya wauzaji wa vyakula vya mifugo kuchanganya vyakula wenyewe bila kufuata utaratibu.
Amesema ni makosa kwa wauzaji wa vyakula vya mifugo kuchanganya vyakula wenyewe na kuwauzia wafugaji na wauzaji wengine kufungua mifuko kutoka viwandani na kuchanganya na vyakula vingine.
Nao baadhi ya wadau walioshiriki katika zoezi la ukaguzi na kuhudhuria kikao hicho jijini Arusha wamepongeza kuwepo kwa ukaguzi wa vyakula vya mifugo ili kuhakikisha vinakuwa bora na kumnufaisha mfugaji ili apate matokeo mazuri ya mifugo yake.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), inatarajia kuendelea kutoka elimu na kufanya ukaguzi wa rasilimali na vyakula vya mifugo katika kanda mbalimbali za wakala hiyo pamoja na kusimamia sheria ili wafugaji ili waweze kufuga kwa tija na kupata matokeo bora kupitia ufugaji.