Afisa mkuu wa Hamas aliitaka Marekani siku ya Jumatatu kuishinikiza Israel kukomesha vita huko Gaza, kabla ya ziara iliyopangwa Jumatatu ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken katika eneo hilo kusukuma mbele juhudi za kusitisha mapigano.
Blinken anatazamiwa kuzuru Misri na Israel siku ya Jumatatu. Pia analenga kuhakikisha vita havienei hadi Lebanon.
“Tunatoa wito kwa utawala wa Marekani kuweka shinikizo kwa uvamizi huo ili kusitisha vita dhidi ya Gaza na vuguvugu la Hamas liko tayari kukabiliana vyema na mpango wowote utakaofanikisha kumalizika kwa vita,” afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri alisema.
Katika ziara yake ya nane katika eneo hilo tangu wanamgambo wa Hamas walipoishambulia Israel mnamo Oktoba 7, na kusababisha tukio la umwagaji damu zaidi katika mzozo wa miongo kadhaa kati ya Israel na Palestina, Blinken pia anatazamiwa kusafiri hadi Jordan na Qatar wiki hii.
Anatazamiwa kukutana na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi mjini Cairo kabla ya kusafiri hadi Israel baadaye Jumatatu, ambako atakutana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, kulingana na ratiba ya Wizara ya Mambo ya Nje.