Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One(AOTL), imewalipa wakulima wenye mikataba na kampuni hiyo jumla ya Dola za Marekani 42,309,297.87 (sawa na 109,164,913,528.81/=) kwa ajili ya kununulia zao la tumbaku.
Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti, amesema pesa hizo zimelipwa tangu kuanza kwa msimu wa ununuzi wa zao hilo ulioanza April 29 hadi sasa.
Amesema pesa hizo zilizolipwa na kampuni hiyo kwa wakulima hao, pamoja na mambo mengine, watazitumia kulipa madeni ya pembejeo walizokopa kutoka benki, halafu kiasi kingine kitakachobaki ndiyo faida yao kwenye kilimo cha tumbaku.
Wakili Magoti amesema kwamba kampuni yake inatarajia kuwalipa wakulima kati ya Dola za Marekani milioni 74.25 hadi milioni 90 mpaka msimu utakapoisha, akiongeza kwamba kiasi halisi cha pesa watakacholipwa kitategemeana na kiasi cha tumbaku ambacho wakulima hao watakavyowasilisha kwenye kampuni hiyo kulingana na mikataba yao ya kilimo kwa msimu huu.
Kwa mujibu wa Wakili Magoti, tofauti na mazao mengine ya biashara, zao la tumbaku linanunuliwa kutoka kwa wakulima kwa kutumia Dola za Marekani, na hivyo zao hilo kuwa moja ya vyanzo vikubwa fedha za kigeni nchini.
Aliongeza kwamba wanunuzi hao kulingana Sheria ya Bodi ya Tumbaku wanalazimika kuwalipa wakulima ndani ya siku 14 baada mauzo kufanyika.
“Hata hivyo kampuni yetu kwa misimu mitatu iliyopita mfululizo imejijengea utaratibu wa kuwalipa wakulima wetu ndani ya siku tano tu baada ya mauzo,lengo likiwa kuwasaidia wakulima, ili waweze wa kulipia mikopo ya pembejeo kwenye mabenki kwa wakati, na hivyo kuwaondolea mzigo wa riba ya kwenye mikopo hiyo, ili kutoathiri faida yao kwenye mapato ya kilimo chao cha tumbaku kwa ujumla,” alisema.
Ameyataja maeneo ambayo pesa hizo zimelipwa, kwamba ni wakulima walioko kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya wilaya za Urambo, Kahama
Sikonge, Kigoma na Kaliua.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Bw Ephraim Mapoore, amesema kampuni yake inatambua kwamba msimu wa zao wa mwaka 2023/2024 haukuwa miongoni mwa misimu mizuri kwa zao la tumbaku kwa wakulima, hasa ikichangiwa uharibifu wa mvua nyingi zilizosababishwa na za elnino, kwani kwa kawaida tumbaku haihitaji mvua nyingi.
Amesema mvua hiyo kwa kiasi fulani imepeleka simanzi kwa wakulima, kwa kuathiri kiwango cha ubora wa zao hilo, pamoja na wingi wa mavuno ya wakulima hao msimu huu.
“Tumeiona hii changamoto iliyowakumba wakulima wetu, na hivyo ili kuhakikisha kwamba wenzetu hawaathiriki kifedha, na pia kutoathiri uendelezaji zao letu sawasawa na sera ya taifa, sisi Alliance One kwa mara ya kwanza tumeamua kutoa motisha ya kifedha kwa wakulima, ambayo inalipwa kwa kila kilo ya tumbaku wanayoiuza,” amesema.
Bw Mapoore amesema kwamba kampuni yake inaamini kwamba motisha hiyo inayotolewa kwa wakulima kwenye msimu huu, itasaidia kuboresha mahusiano kati ya kampuni na wakulima, lakini pia itasaidia kukuza kwa sekta ya ndogo ya tumbaku, pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kiongozi wa Chama cha Msingi cha Twende Pamoja Amcos, Ramadhan Kisena, kilichopo Kijiji cha Kalunde kilichopo wilaya Tabora Mjini na ambapo kina mkataba na kampuni ya Alliance One, akiongea kwa niaba ya wakulima wenzake amesema wamefurahia sana bei ya tumbaku mwaka huu na kwamba hawana mpango wa kuachana na kampuni hiyo.
“Tunaipongeza serikali kwa kuruhusu kuongezeka kwa wanunuzi wa zao hili nchini,kwani mashindano yao yamekuja pamoja na ongezeko la bei ya zao,kwani imeleta msukumo mkubwa kwa wakulima kupanua mashamba yao na hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa kuikuza sekta yetu” amesema.
Amesema huku wakishawishiwa na ongezeko kubwa la bei msimu huu, wanachama wa chama chake wamefanikiwa kuongeza uzalishaji hadi kilo 700,000, ambapo kati ya hizo tayari wamefanikiwa kuuza kilo 240,000, ambazo tayari wamelipwa zaidi ya shilingi bilioni, akiongeza kwamba wana uhakika watauza zao lote lilibaki.
Akifafanua amesema, msimu wa mwaka 2021/22, wanachama hao walivuna kilo 350,000, wakati msimu wa mwaka 2022/2023 walivuna kilo 580,000.Amesema mafanikio yao yanatokana na kuvutiwa na bei nzuri pamoja na utayari wao kupokea mafunzo ya kilimo wanayopewa na maafisa kilimo kutoka kampuni ya Alliance One.
“Sababu zingine za mafanikio yetu ya kupata madaraja mazuri ya tumbaku ambayo yanauzwa kwa bei nzuri ni kujenga mabani mazuri ya kukaushia zao, hili pamoja na kukausha tumbaku kwa kutumia miti yetu ya kupandwa nasisi wenyewe, lakini pia kuhifadhi vizuri tumbaku iliyokaushwa,yote hayo yakiwa ni mafundisho tuliyofundishwa na Alliance One,” alisema.
Kuhusu tabia ya kuchanganya tumbaku na bidhaa zingine ambazo ni tofauti na zao hilo, ili kuliongezea uzito na kupata kilo nyingi wakati wa mauzo,tatizo ambalo limesambaa miongoni mwa wakulima wengi, Bw Kisena amesema kwe chama chake hawana tatizo hilo kwa sasa, baada ya kufanikiwa kupambana nalo na kufanikiwa kulimaliza.
Kwa upande wake, Katibu Meneja wa Chama hicho cha Twende Pamoja Amcos Subira Salum amesema kwa msimu huu kampuni ya Alliance One tayari imelipa pesa kwa kilo 240,000 walizouza na tayari pesa zimeingizwa kwenye akaunti yao, akiongeza kwamba nab ado wakulima wanaendelea kupeleka mavuno yao kwenye kampuni hiyo kwa ajili ya mauzo.
“Bei ya wastani kwa msimu huu ni Dola ya Marekani 2.4 kwa kilo moja, halafu safari hii kampuni inatuzawadia shilingi 102/= kwa kila kilo ya tumbaku tunayowauzia kama motisha na asante yao kwetu,” amesema.
Amesema kutokana na habari njema iliyoletwa kijijini hapo na kampuni ya Alliance One, chama chake cha msingi chenye wanachama 350, sasa kinapata maombi ya wanachama wapya kila uchao kutoka kwa wanakijiji cha Kalunde ili na wenyewe wajiunge kulima zao hilo ambalo siyo wanakijiji wote wanalima kwa sasa.